Katika Hip Hop ya Tanzania utakosa fadhila kama hutotaja vijana wa mwanzo kabisa ambao kuanzia mivao yao na kufoka foka kwao kulikuwa ni burudani na ushawishi tosha kwa watu kuanza kudadisi kuhusu maana halisi ya utamaduni huu hasa Tanzania.Kwa wakati huo ilionekana kama uhuni tena wa kupita kiasi.Nitawataja wachache ninaowakumbuka ambao kila kukicha ukigongana nao kwenye Night Clubs,Samora Avenue pale Salamander basi ulikuwa unachoka mwenyewe.Nakumbuka vijana kama
John Simple,
Dj Rusual,
The BIG One,
Babu Manju,
David Nhigula,
Abdulhakim Magomelo,
Kessy,
Ibony Moalim,
Tom London,
OPP (now Jay P) na
Dj Ngomeley.
Tukiendelea hao niliowataja hapo juu walikuwa chachu katika uvaaji wa kihip-hop na katika kughani na sijui kama kuna mtu atasahau watu kama Fresh XE Mtui,BBG (alianza na Mr II),Adili kumbuka,KBC (Mbeya Tech),Saleh Jabir,Samia X,THE BIG,Rhymson,2Proud.Deplowmatz na wengineo wengi ambao walikuwepo na wakighani katka school parties au matamasha ya mtaani kabla hata ya kurekodi nyimbo zao studio.
Kwa mara ya kwanza pia promoters kama Joe Kusaga na Abdul hakim Magomelo walionekana kutobaki nyuma katika ukuzaji wa sanaa hii ambapo waliandaa matamasha mbali kama Yo! Rap Bonanza na Coco beach Bottle Parties kwa ajili ya kuwapa nafasi wale wenye uwezo wa kughani.Matokeo yake yalikuwa ya kufurahisha kwani kila mmoja alikuwa na shauku ya kuingia katika gemu.
Kwa vile sio watu wote walikuwa na uwezo wa kughani lakini pia kulikuwa na wale wenye kuimba kama wanamuziki wengi wa Marekani kwa kupitia matamasha mbali mbali kwenye Jumba la utamaduni la Urusi,Korea na mengineyo yalikuwa yakiandaliwa hasa na wanafunzi wa shule mbali mbali za sekondari jijini kama Forodhani pia matamasha yaliyokuwa yakifanyika kando kando ya ufukwe ambako wengi wenye kutaka kuimba walijitokeza.Hapa tunakumbuka kundi kama la Mawingu na mwana dada Pamela,mwanadada Stara Thomas na Judith Wambura ambao uwezo wake wa kughani na kuimba kama Mc Lyte ulimpa tafu hasa alipofanya hivyo kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha DJ show ya Radio One,shukrani kwa Ipyana Malecela Mkwavi (RIP) kwa zawadi ya LP yenye instrumental (ala) tupu aliyonipatia kama zawadi aliporudi toka UK kwani instrumental ya single “Keep,Keeping on” ndiyo iliyomtambulisha Jay Dee wa leo Radioni kwa mara ya kwanza japokuwa kabla ya hapo alikuwa mwimbaji wa kwaya kanisani lakini mweye kusita kuingia kwenye muziki wa kidunia.Pia Kundi la R&B lililojulikana kama Four Krewz Flava pia Herbert Makange ambaye pia alikuwa akiimba.
Naweza nikawa nimesahahu majina machache hapo juu lakini kwa ufupi hao ni baadhi ya watu wa mwanzo kabisa kuuingiza masikioni mwa jamii muziki wa kizazi kipya pengine hata kabla ya chombo kilichoipaisha juu zaidi..RADIO.Na ninaposema Radio simaanishi Radio nyingine bali Radio One Stereo kama Radio pekee yenye kujivunia juu ya ukuaji wa muziki huu wa kizazi kipya kufikia hapa ulipo.
Lakini uko nako hakukuwa na mteremko,mambo yalikuwa mengi na mazito mpaka muziki kujipenyeza na kukubalika.Je nini kilichochea mapambano ya kuuchomeka muziki huu Radioni na kuupa nafasi ya kupigwa sambamba aina zingine za muziki kama ule wa dansi nk? nani alihusika katika harakati hizo na nini kilifuata? ugumu huo ulitokana na nini?
Lakini mimi binafsi mbali ya mkongwe Taji Liundi ambaye alifungua njia ya mapambano na harakati ili kuupa muziki huu nafasi yake kama ilivyo dansi na aina nyengine ya muziki,kamwe sitomsahahukijana mwenye akili “Genius” Dj Sebastian Maganga ambaye alipokea kwa dhati mikoba ya DJ SHOW baada ya miye kuachia ngazi.Sebastian ana nafasi ya pekee sana katika muziki huu tangu alipojiunga na Radio One toka Radio Tumaini,ikumbukwe pia Sebastian ni mwana HipHop aliyetoka na kundi la Afro Reign toka miaka hiyoo.Sebastian ni mbunifu na ndio yeye aliyenisukuma zaidi katika kuibadili DJ Show moja kwa moja na kuachana na nyimbo nyingi za Marekani katika kipindi cha DJ SHOW na pole pole tuliweza kufanikiwa kwa kushirikiana na DJ Jumanne kutoka Holland ambaye alitutengenezea promo nyingi za kipindi na kubadili usikivu wa kipindi hiki kutoka muziki wa Snoopy Dogg/Dr Dre mpaka ule wa akina Mr II/Kwanza Unit.
Na katika kufanikisha hilo kwa vile DJ Show ilikuwa inapiga muziki mchanganyiko lakini wa kileo.Siku moja tukiwa kwenye kipindi Sebastian aligusia mfumo wa kutenga muziki katika dakika 30 kila genre,kama tunapiga Reggae basi alishauri iwe dakika 30,kama R&B ya Tanzania basi tutenge dakika 30 nk.Nilikubaliana na wazo hilo kwani lingetufanya tutoe nafasi sawa kwa kila aina ya mtindo na sio upendeleo wa kupiga Hip Hop au R&B tu masaa yote mawili ya kipindi.
Ilipofika dakika 30 za muziki wa R & B,siku hiyo nilikuwa kwenye usukani na kwa mbwembwe nilicheza nyimbo ya kundi la R&B lililoitwa 4Krewz Flava na baadaye kuiunganisha na nyimbo nyingine ya Unique Sistaz.Kwa vile midundo,mpangilio,lugha na utaalamu wa muziki wenyewe kamwe huwezi kuufananisha na ule wa Soul 4 Real au SWV kutoka Marekani,tulipenda tutofautishe kidogo kati ya aina hizi mbili na ndipo session hii niliibatiza jina ambalo lingetofautisha R&B ya Marekani na ile ya kwetu….niliipa session hii jina la
BONGO FLAVA.Hii ilikuwa mwaka 1996 na ndio ulikuwa mwanzo wa neno BONGO FLAVA likiwa na maana muziki wenye mahadhi ya nje lakini wenye vionjo na ladha ya Tanzania na si vinginevyo lengo kuu ni kuitofautisha na muziki ule wa Marekani.Hip Hop ya Tanzania ilibaki na itabaki vile vile kama ilivyo,ila muziki wowote ule wa nje,mbali ya Hip Hop na DANSI ya Tanzania niliuita na kuufahamishakwa umma wa watanzania kama BONGO FLAVA ndani ya kipindi cha DJ SHOW cha Radio One.
Nikifikia tamati ya mtazamo wangu na jinsi nilivyoshuhudia muziki huu ukikua pengine kumekuwa na ubishi ambao kwa maana halisi nimeonelea nao niudodose kidogo hii leo.Nilipokuwa nyumbani Tanzania nilipata bahati ya kutembelea Clouds FM ambako mwenzangu Sebastian Maganga sasa ni Mkuu wa Vipindi na aligusia suala hili la chimbuko zima la muziki huu na neno BONGO FLAVA.Niliweka haya unayoyasoma wewe hapa bloguni kama yalivyo na niliomba yeyote mwenye kuona tofauti na ninauona ukweli kujitokeza lakini hakutokea mtu kupinga.
Nasema hivi kwa vile huko nyuma kuna waliodiriki kujitokeza/kujitangaza hapo mwanzo na kudai kuwa neno hili BONGO FLAVA ni jina lililotokana au kutungwa na wao,kitu ambacho mimi na mwenzangu Sebastian Maganga tunakipinga kwa sababu tunajua ukweli uko wapi.Watu hawa (tunafahamiana fika) waliombwa kuja studio za Clouds FM siku hiyo katika mahojiano maalum na kuuthibitishia umma juu ya dai lao lakini hakuna aliyetokea.
Ni kweli kila mtu na mtazamo wake katika kila jambo kutokana na alivyolishuhudia lakini ni vyema tukawa wakweli kidogo bila kupindisha mambo pale tunapotaka kuuhabarisha umma juu ya yale tunayotaka wayafahamu.Katika mnyambulisho huu hapa juu sio lengo wala nia yangu kumsuta mtu na inawezekana kabisa kama binadamu wa kawaida kuna mambo nimeyasahau,kama ndivyo basi ni vyema tukasahihishana ili kurekebisha mambo na sio kudanganya kwa kudhani ukweli kamwe hautojulikana na ndio maana nimeamua kuandika haya ili kuweka yale ninayoyajua wazi kwa faida ya kizazi kijacho na hata cha sasa ambacho kimekuwa kikipotoshwa na wachache.
Na kwa kufanya hivi sina nia hata kidogo ya kutaka au kuuukwa umaarufu,kwani nimekuwa maarufu toka nina miaka 19 na sihitaji wala silazimishi kuwa maarufu hivi leo.
Ieleweke kuwa haya yote ni katika kutoa elimu kama shuhuda wa mapinduzi ya muziki huu Tanzania kwani kumekuwa dhahiri na upotoshaji wa makusudi au wa kutojijua inapokuja katika mambo muhimu yanaohusu muziki wa kizazi kipya Tanzania.
Kwa mfano neno hili la BONGO FLAVA lilizaliwa na kutokea katika kipindi cha DJ Show na si vinginevyo kama ambavyo imekuwa ikidaiwa katika zinazoitwa historia za muziki huu wa kizazi kipya kutoka vianzio mbali mbali.
Mfano mwingine hai ni ule kuwa kuna kuna wanaosema TANZANIA MUSIC AWARDS imeanzishwa na mwanamuziki James Dandu (ambaye alikuwa ni rafiki yangu mkubwa) lakini watu wanasahau kuwa TANZANIA MUSIC AWARDS ilianzishwa na mwanamuziki wa zamani wa bendi ya Mawenzi/Prodyuza John Kagaruki chini ya kampuni yake ya Serengeti Production kwa kushirikiana na BASATA mwaka 1997 na sherehe za kwanza kabisa ambazo zilirushwa live na kituo cha ITV zilifanyika pale Whitesand Hotel.
Ni kweli mwaka uliofuata sherehe hizi hazikufanyika tena na zilipwaya.Lakini tusisahau kuwa mwaka 2000 kampuni ya Look Promotion kwa kushirikiana na Clouds FM walifanya tena onesho hili ikiwa ni mara ya pili kufanyika Tanzania.Na mwaka uliofuata bia ya Kilimanjaro kwa kushirikiana na mwanamuziki James “CJ MASSIVE” Dandu na kampuni yake ya Dandu Planet walizindua upya sherehe hizi ambazo zimekuwa zikifanyika kila mwaka toka wakati huo.
Mifano kama hii na mingineyo mingi tu inaleta mushkeri hasa inavyopotoshwa kwa makusudi ilhali mashuhuda wake tupo tena tukiwa hai.
Ebwaneeeeeeeeeeee issue ndio iko hovyooo.ni kwa mujibu wa
MIKE MHAGAMA.